Wednesday, 19 July 2017

MAISHA YA NDOA

SABABU 4 ZA KIBIBLIA ZA KUINGIA KWENYE NDOA.

NDOA sio wazo la mwanadamu bali ni wazo la Mungu. Baada ya Mungu kuona mwanaume amekuwa mpweke akasema si vema mtu huyu awe peke yake ndipo akaamua kumfanyia msaidizi wa kufanana naye. Kwa hiyo ndoa ni taasisi ya kwanza duniani kuanzishwa na Mungu mwenyewe. Ili tuweze kuielewa vizuri misingi au sababu za kuwepo kwa ndoa lazima tuangalie Biblia inasema nini.

1.KUPATA RAFIKI WA MAISHA

Bwana Mungu akasema, Si vema huyo mtu awe peke yake…

Mke ni rafiki na mke kwa agano (Malaki 2:14) kwa hiyo juu ya yote ndoa ni urafiki. Kiukweli huwa nafarijika ninapoona wanandoa wenye miaka mingi wakitembea njiani pamoja kama marafiki. Kumbuka jambo hili rafiki yangu, cheti cha kanisani kinaweza kumfanya awe mume/mke wako lakini hakina uwezo wa kumfanya awe rafiki yako, lakini ujue Mungu anakupa mke ili usiwe mpweke, yaani kumbe kusudi la ndoa ni kujipatia mtu wa karibu wa kupiga naye stori na kumshirikisha mambo yako.

Kwa hiyo swali sio “Je ataweza kunilea?” au “Je atanilinda?” badala yake swali la kwanza kabla hujaoa au kuolewa unalopaswa kujiuliza ni hili, “ Je atakuwa rafiki yangu wa karibu?” au “Je nimejiandaa kuwa rafiki yake wa karibu?” yaani atakuondolea upweke?

MWANZO 2:18.

2.ILI KUPATA MSAIDIZI

Bwana Mungu akasema, Si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye.

MWANZO 2:18.

MKE NI MSAIDIZI: Mke anamsaidia mume kwa kumuombea, kumpa penzi, kumpa chakula, kumshauri, kumsaidia kazi za nyumbani, kumsaidia malezi ya watoto, kumfariji, kumsaidia shughuli za kiuchumi, shughuli za kijamii nakadhalika pamoja na huduma/kazi ambayo Mungu amempa ili kutimiza kusudi.

3.ILI KUTOFANYA ZINAA

Lakini kwa sababu ya zinaa kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke na awe na mume wake mwenyewe.

1 Wakorintho 7:2

Kuna watu wanafundisha kwamba usioe au kuolewa kwa sababu ya tamaa za kimapenzi lakini Biblia inasema wazi kuwa kama unasumbuliwa na shauku za zinaa ni afadhali ukaamua kuoa au kuolewa kuliko kuingia kwenye uasherati na kutenda dhambi.

Lakini ikiwa hawawezi kujizuia, na waoe; maana ni afadhali kuoa kuliko kuwaka tamaa.

1 Wakorintho 7:9

4.ILI KUPATA WATOTO

Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi.

Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba.

Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi.

Mwanzo 1:26-28

ANGALIZO:

Kupata watoto sio kigezo cha kuthibitisha uhalali wa ndoa; Na kukosa watoto sio sababu ya kubatilisha ndoa kwa sababu ndoa ni kati ya mume na mke walioamua kuishi pamoja.

 

HITIMISHO

Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu.

Waebrania 13:4

No comments:

Post a Comment

Comments system

KATEMBO JR BLOG

J.P. KATEMBO

JACKSON PHOCUS KATEMBO