Watoto wanapofikia hatua ya kubalehe na kuvunja ungo familia inapitia mabadiliko ya lazima kwenye maeneo mengi lakini kwa sababu BALEHE SIO TATIZO lazima tutegemee mabadiliko hayo ambayo kimsingi yanaweza kuleta furaha au msongo wa mawazo na hali ya kukosa utulivu nyumbani. Kwa hiyo kutokana na mabadiliko hayo ni lazima kukubaliana juu ya utaratibu wa mahusiano mapya kati ya wazazi na watoto pia kati ya mke na mume. Yafuatayo ni baadhi ya mapendekezo ili kuendelea kuwa na familia imara wakati watoto wanapitia kipindi cha balehe.
1.BADILI AINA YA MALEZI.
Balehe ni kipindi ambacho mtoto anafikia hatua ya kutaka kujiongoza kwa hiyo hahitaji kuamriwa na kufundishwa sana. Kwa hiyo wanahitaji msaada mdogo tu kwenye masomo yao, wajibu wao na mafundisho mengine lakini kwa bahati mbaya wazazi wengi hawako tayari kupunguza mamlaka yao. Tabia ya kumlea kijana wako aliyebalehe kama vile bado mtoto mdogo haina mafanikio ya kweli, anaweza kukutii machoni pako lakini akafanya mambo ya ajabu akiwa mbali na wewe. Huu ni wakati wa kupunguza amri na kuonesha kwamba unatambua kwamba amekomaa lakini unabaki kuwa mshauri wake mkuu. Japokuwa fimbo ni nzuri lakini haishauriwi kutumia fimbo wakati huu. Badala ya kuondoa ujinga ndio kwanza atajenga uadui na hawezi tena kukusikiliza kwa lolote.
2.KUBADILIANA NA MABADILIKO YAKE YA KISAIKOLOJIA.
Hiki ni kipindi ambacho mtoto anakuwa mbishi yaani anapenda mashindano kwa sababu anajiona amekuwa. Hata hivyo ni lazima uwe makini kwa sababu usipokuwa makini anaweza kufikia hatua ya kuwadharau wazazi na kuwatukana (mara nyingi haya huwa ni matokeo ya malezi mabaya hata kabla mtoto hajabalehe).
3.MPE TAHADHARI KWENYE TABIA HATARISHI.
Balehe huambatana na tabia nyingi hatarishi kama vile ngono, madawa ya kulevya, punyeto, ugomvi, wizi, tabia za ajabu, ukosefu wa maadili kwa walimu nakadhalika. Mpe tahadhari mapema kwa kumweleza matokeo ya tabia hizo bila kumficha lolote. Usimwonee aibu kwa sababu wakati huu kijana atatamani kujaribu karibia kila kitu.
4.JIANDAE KUKUBALIANA NA MABADILIKO YAKE YA KIHISIA.
Wakati wa balehe watoto wengi wanaona wazazi wao ni kero. Kwa lugha nyepesi wanaona wanaonewa, wanasumbuliwa, wanabanwa nakdhalika. Mzazi unaweza kumkataza mtoto asifanye jambo fulani kwa lugha nzuri tu lakini mtoto akasema, “Mbona unanigombeza?” hii ni kwa sababu balehe inampa hisia za kuona wazazi wanataka kumtawala wakati yeye anaweza kujitawala. Usimkatie tamaa na kumpa uhuru uliopitiliza lakini pia utambue hiki ni kipindi kifupi kitapita.
5.IFAHAMU NGUVU YA MARAFIKI.
Hii si taarifa nzuri sana kwa mzazi; Unajua kuwa kipindi cha balehe mtoto anawasikiliza zaidi marafika/makundi rika kuliko wazazi/walezi? Ndio! Kwa kujua hilo itakusaidia kuelewa umuhimu wa kujenga urafiki na kuwafahamu marafiki zake pia ili akiwepo wa kuharibu tabia uweze kuwapa tahadhari na kuwaonya mapema.
6.RUHUSU MALEZI YA KIUTU-UZIMA KUTOKA KWA WATU WENGINE.
Kwa sababu mtoto ana mtazamo kwamba wazazi mnamtawala au mnambana ni vema ukamruhusu mtoto wako kukutana na walimu wengine ambao atawasikiliza kama vile semina za vijana kanisani, walimu shuleni au rafiki wa familia ambaye unajua mtoto wako anampenda na kumheshimu. Wakati mwingine mtoto hawezi kusema mambo yanayomsumbua lakini kwa watu hao akasema na kusaidiwa.
7.MSHIRIKISHE KWENYE MAAMUZI YA KIFAMILIA.
Wape nafasi watoto wako kutoa mawazo na mapendekezo yahusuyo familia lakini maamuzi ya mwisho yanabaki kwa wazazi. Hii ni njia mojawapo ya kudumisha umoja wa kifamilia na kumfanya mtoto ajue kwamba unaamini akili yake kwa hiyo haitakuwa rahisi kwake kufanya maamuzi ya hasara kwenye mambo yake kwa sababu anajua wazazi hawategemei hasara kutoka kwake
©CHOIJACK
No comments:
Post a Comment